Kiungo Geita: Simba wamekuja

 SIMBA wameanza kuweka mipango sawa ya kusajili dirisha dogo, yapo majina yanatajwa kujadiliwa kwenye vikao vyao ili kukiboresha kikosi hicho na nje na Ligi Kuu Bara kina majukumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kati ya majina hayo, kuna jina la kiungo mkabaji wa Geita Gold, Kelvin Nashon ambaye halikuanza kutajwa leo wala jana ni tangu dirisha kubwa hata watani wao wa jadi Yanga waliwahi kuisaka saini yake miaka ya nyuma.

Mwanaspoti likamnyanyulia simu kupata uhakika wa taarifa hizo, baada ya kupenyezewa za ndani na vigogo wa Simba ili kuwalete muendelezo wa kile kinachoendelea

Nashon alikiri kuwepo na mazungumzo baina yake na viongozi wa Simba ingawa hakutaka kuyaelezea kwa kirefu akidai kuna hatua zinatakiwa kufuatwa kwani yeye ni mali ya Geita Gold.

“Nilipigiwa simu na mmoja wa kiongozi wa Simba, ila siwezi kuelezea sana tulizungumza nini kwa sababu haya mambo yana hatua zake, nimekupa ushirikiano baada ya kuona taarifa zangu zipo hewani.

Alipoulizwa kama ni kweli hata Yanga imewahi kuhitaji saini yake? Alijibu “Kipindi cha nyuma, ninachoamini kila jambo lina muda wake, kikubwa ni kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia miiko ya kazi.”

Bado Mwanaspoti likataka kujua mambo mengi kutoka kwake, akaulizwa kwa mara nyingine vipi kuhusu nafasi yake kabla ya kukubali ofa ya Simba? Alisema anaheshimu kila mchezaji pia anapenda ushindani.

“Kila mchezaji ana kitu chake ambacho anakifanya kwa ubora wa juu, hivyo endapo kama dili likitiki, najua uwezo wa Jonas Mkude, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin ni wachezaji wazuri na wanaisaidia timu yao,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.