Akamatwa kwa kuuza viungo vya maiti

Mmiliki wa zamani wa chumba cha kutunzia maiti (Mochwari) katika Jimbo la Colorado, Marekani, amehukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kuwalaghai ndugu wa waliofariki na kuuza viungo vya miili ya maiti 560 bila idhini.

Megan Hess, 46, aliungama makosa ya ulaghai mnamo Julai 2022, akiendesha hifadhi ya maiti ya Sunset Mesa. Hess pia alikuwa anamiliki shirika la kutoa huduma za mchango wa viungo vya mwili kutoka jengo moja mjini Montrose, Colorado. Alihukumiwa kifungo cha miaka 20 mnamo Jumanne, Januari 3, ambacho ndicho kinaruhusiwa chini ya sheria ya taifa hilo.

Mama yake Hess, mwenye umri wa miaka 69, Shirley Koch, pia alikiri kosa la ulaghai na alihukumiwa kifungo cha miaka 15, Mahakama iliambiwa kuwa jukumu kuu la Koch lilikuwa kukatakata miili. "Hess na Koch walitumia mochwari yao wakati mwingine kuiba miili na viungo vya mwili kwa kutumia fomu za wafadhili za ulaghai na ghushi," mwendesha mashtaka Tim Neff aliambia mahakama akiongeza kuwa tabia ya Hess na Koch ilisababisha uchungu mkubwa kwa familia za waathiriwa.

Hakimu wa Wilaya ya Marekani Christine M. Arguello akitoa uamuzi wake alisema kuwa kesi hiyo ilikuwa ya kuhuzunisha zaidi ambayo hajawahi kukumbana nayo mahakamani, hivyo hakimu huyo aliamuru kwamba Hess na Koch wapelekwe gerezani mara moja.

Katika mochwari yake, Hess alikuwa akitoza familia hadi $ 1,000(Zaidi ya Milioni 2 za kitanzania) akiwalaghai kuwa ni gharama ya uchomaji wa maiti ambao haujawahi kutokea. Waendesha mashtaka walisema alidanganya zaidi ya familia 200, ambazo zilipokea majivu yaliyochomwa kutoka kwa mapipa yaliyochanganywa na mabaki ya maiti tofauti.

Ni kinyume cha sheria nchini Marekani kuuza viungo vya mwili kama vile mioyo na figo kwa ajili ya kupandikiza, Lakini kuuza sehemu za mwili kama vile vichwa, mikono na uti wa mgongo kama alivyofanya Hess, kwa matumizi ya utafiti au elimu, hakudhibitiwi na sheria.

Chanzo: Mtandao

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.